Skip to main content
UDSM-wanahabari-Kiswahili

MASIKIDU 2024: UDSM yawafunda wanahabari, yaendesha Mjadala kabambe wa Kiswahili

Na Jackson Isdory, CMU

Katika kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU), tarehe 7 Julai, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka huu 2024 kimetoa mafunzo maalum kwa wanahabari juu ya matumizi ya Kiswahili na kuendesha Mjadala wa kitaaluma wa wadau kuhusu lugha hii adhimu.

Mafunzo kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili, yaliyoendeshwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kama sehemu pekee ya maadhimisho haya ya Siku ya Kiswahili, yaliwaleta pamoja wanahabari wa vituo vya televisheni, redio, magazeti, na wale wa mitandaoni pamoja na maafisa habari wa taasisi za serikali na binafsi.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Juni 2024, Rasi wa Ndaki ya Insia, Profesa Rose Upor, ambaye alimwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Utafiti, Profesa Nelson Boniface, alihimiza ushirikiano wa chuo na wanatasnia katika maendeleo ya nchi hasa katika utamaduni na kukuza lugha hususani matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za kila siku.

“Mafunzo haya yanalenga kuhimiza kila mmoja wetu kuzingatia umuhimu wa matumizi sahihi ya msamiati na istilahi za Kiswahili, pamoja na kuzingatia maadili katika utangazaji wa Habari”, alisema Prof. Upor. 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI), Prof. Shani Omari Mchepange, alieleza malengo ya mafunzo hayo, akibainisha namna idadi ya waombaji wa mafunzo ilivyokuwa kubwa. Alisisitiza pia umuhimu wa kuendeleza mafunzo hayo hata baada ya MASIKIDU.

“Mafunzo haya ni bure kwa kila mshiriki kama sehemu ya mchango wa UDSM katika kuadhimisha MASIKIDU kwa mwaka 2024. Huu ni mwendelezo wa juhudi za Chuo katika kutoa huduma kwa jamii. Tunaamini kuwa tutaendelea kushirikiana ili kuboresha matumizi ya lugha ya Kiswahili”, Prof Mchepange alitanabaisha.

Mada na Wakufunzi

Mafunzo hayo yalikuwa na mada mbalimbali kuntu kwa wanahabari zilizotolewa na nguli wa Kiswahili hasa katika taaluma ya habari. Miongoni mwao ni Dkt. Titus Mpemba, Mhadhiri wa TATAKI, aliyefundisha kuhusu ‘Matumizi ya Lugha katika Uandishi na Utangazaji wa Habari’ akiangazia utumizi wa sarufi ya Kiswahili sanifu na fasaha, mbinu za uandishi, na kuondoa makosa ya kisarufi katika habari.

Mwingine ni Dkt. Victor Eliah, mtangazaji wa TBC1, aliyefundisha kuhusu Uhusiano wa Vyombo vya Habari na Maendeleo ya Lugha ya Kiswahili, Uhusiano na Ushirikiano baina ya Vyombo vya Habari na Asasi nyingine za Kiswahili, na Teknolojia, Changamoto, na Fursa za Kiswahili katika Vyombo vya Habari.

“Washiriki walijifunza nadharia na vitendo kwa kuchunguza na kusahihisha makosa ya kisarufi yanayotokea katika vyombo vya habari. Walipendekeza kuwa mafunzo hayo yawe endelevu na yapelekwe katika mikoa mingine ili kuwafikia wanahabari wengi zaidi,” alisema Dkt. Mpemba.

Bi. Theresia Mmasy, Meneja Uhusiano wa Kampuni ya ALAF iliyofadhili mafunzo hayo aliipongeza UDSM kwa juhudi zake katika kuendeleza lugha ya Kiswahili. “Kampuni ya ALAF imejizatiti kufadhili shughuli na makongamano ya lugha ya Kiswahili pamoja na wanafunzi wa masomo ya Kiswahili ngazi ya Umahiri katika Chuo hiki ili kuidumisha lugha hii adhimu, kuiendeleza na kuieneza kote duniani”.

Mjadala Maalum wa Kiswahili

Katika hatua nyingine, UDSM kilifanya mjadala maalum wa Kiswahili tarehe 3 Julai, 2024 kikishirikiana na wadau wakuu wa Kiswahili kama vile Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Lengo kuu la mjadala huo lilikuwa kujadiliana kuhusu ‘Uzoefu wa Nchi za Nje katika Ufundishaji wa Kiswahili’. Nchi zilizohusika katika kuwasilisha makala za mjadala ni Ufaransa, Urusi, Italia, Misri, Austria, Ghana, Burundi, Zimbabwe na Uganda.

Akifungua mjadala huo wa kitaaluma, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, alisifu mchango wa viongozi wa serikali katika mafanikio ya kukua kwa lugha ya Kiswahili na kupongeza ushiriki wa wadau mbalimbali wa Kiswahili katika mjadala huo.

“Lugha ya Kiswahili imeenea duniani kote na sasa ni lugha ya kimataifa. Nawashukuru waandaaji wa mjadala, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) kwa kusimamia vyema tukio hili”, alisema Balozi Mbarouk.

Alisisitiza umuhimu wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kukiendeleza Kiswahili na kujadili changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kwa wageni. Alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kujisajili katika kanzidata ya BAKITA na BAKIZA ili kurahisisha upatikanaji wa wataalamu wa Kiswahili wakati wa mahitaji.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William A. L. Anangisye aliyewakilishwa na Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia, Prof. Flora Magige, alieleza furaha ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa mjadala huo na kusisitiza umuhimu na mawanda ya kaulimbiu ya MASIKIDU ya mwaka huu ambayo ni ‘Kiswahili na Fursa za Maendeleo Duniani’.

“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanzisha mipango kadhaa ya kukuza Kiswahili, ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Afrika na kutumia Kiswahili kama lugha rasmi katika mikutano yote hapa chuoni. Tunatoa wito kwa washiriki kujadili fursa za ufundishaji Kiswahili nje ya nchi”, alibainisha Prof. Magige.

Mkurugenzi wa TATAKI, Profesa Shani Omari Mchepange alieleza namna maadhimisho ya mwaka huu yalivyodhihirisha hadhi na nafasi ya lugha ya Kiswahili duniani na mchango wa vyuo vikuu nchini katika maendeleo ya lugha hiyo.

Katika MASIKIDU ya mwaka 2024, UDSM imeonyesha kwa mara nyingine tena kuwa ni nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili duniani. Maadhimisho haya ya Siku ya Kiswahili Duniani yameacha alama thabiti na kutoa matumaini makubwa kwa mustakabali wa Kiswahili kama lugha ya kimataifa.