Profesa Anangisye: Tutaendelea Kuyaenzi Mageuzi ya Kitaasisi Aliyoasisi Profesa Luhanga
Mawasiliano na Habari, UDSM
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amesema kuwa Chuo kitaendelea kuyaenzi kwa weledi na umuhimu mkubwa mageuzi ya Kitaasisi aliyoyaasisi aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo hiki kuanzia mwaka 1991 hadi 2006, Hayati Profesa Matthew Luhanga.
Profesa Anangisye ameyasema hayo wakati wa ibada na itifaki ya kitaaluma ya kumuaga Profesa Luhanga katika Ukumbi wa Nkrumah siku ya Jumatatu tarehe 20 Septemba mwaka huu; ambapo ibada nyingine na mazishi ilikuwa siku ya Jumanne tarehe 21 Septemba 2021, Bahari Beach, Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Anangisye ameeleza kuwa chini ya uongozi wa Profesa Luhanga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipata mafanikio makubwa pamoja na ukweli kwamba aliingia madarakani wakati ambapo nchi na Afrika kwa ujumla ilikuwa inapitia kipindi cha mageuzi.
“Wakati huo nchi ilikuwa inaingia katika mfumo wa siasa wa vyama vingi na kulikuwa na harakati nyingi za kutaka mabadailiko mengi ya kisera ikiwemo ile ya kuchangia huduma za elimu ya juu,” alisema Profesa Anangisye.
Profesa Anangisye ameongeza kwamba, kwa kuwa ilihitajika uongozi mahiri ili kukivusha Chuo katika kipindi hiki, Profesa Luhanga alijidhihirisha kama nahodha asiyetetereka “hata wakati wa mawimbi makali ya bahari yaliyokuwa yanavuma wakati huo”.
“Mojawapo ya kazi alizofanya wakati wa uongozi wake ni pamoja na kuanzisha na kusimamia Programu ya Mageuzi ya Kitaasisi (Institutional Transformation Programme-ITP). Mageuzi yaliyokiwezesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa cha karne ya 21”, amesisitiza Profesa Anangisye.
Ni kwa muktadha huo, amesema, Chuo kitaendelea kudumisha na kusimamia miradi na mipango yote iliyoanzishwa na ITP kwani ndio imekuwa chimbuko la mafanikio makubwa yaliyopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na elimu ya juu nchini Tanzania kwa ujumla.
Profesa Anangisye amesema kuwa Profesa Luhanga atakumbukwa sana pia kwa kuwa imara katika kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwa juhudi zake kumekuwepo kupanda mishahara ya wafanyakazi na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi-maarufu kama Nyumba za Mwinyi.
Viongozi na watu wengine waliohudhuria ibada hii ya kumuaga Hayati Profesa Luhanga, iliyotanguliwa na maandamano ya kitaaluma kwa heshima yake, walimuelezea kuwa alikuwa kiongozi mahiri, mwenye msimamo usiotetereka, mfuata utaratibu, mwenye maono na mchapakazi, mwanataaluma mahiri, mzalendo wa kweli, aliyeipenda familia yake na nchi yake kwa dhati, na aliyejali kukuza vipaji vya wengine hasa vijana.
Viongozi hawa ni pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo (Mb.) aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mstaafu, Dkt. Mohamed Ali Shein aliyeambatana na viongozi wengine waandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Pia alikuwepo Mkuu wa Chuo Kikuu Sokoine cha Kilimo na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba; Jaji Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Barnabas Samatta; Mwakilishi wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu, Prof. James Mdoe na viongozi mbalimbali kutoka Wizara hiyo, Viongozi Waandamizi wa Serikali, wawakilishi wa Mashirika mbalimbali, viongozi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu.
Aidha, Profesa Anangisye aliwasilisha pia salamu za pole kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye hakuweza kufika kumuaga Prof. Luhanga kutokana na sababu zisizozuilika. Rais Mstaafu Kikwete amesema “ningetamani kuwepo kumsindikiza mtu tumefahamiana kwa miaka mingi na kufanya naye kazi”.
Pia, Profesa Anangisye alitoa salamu za pole kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Jaji Mstaafu Damian Lubuva ambaye alieleza kuwa Baraza linaahidi kuenzi na kufanyia kazi mawazo ya Profesa Luhanga na litamkumbuka sana mtu huyu “ambaye ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam”.