Skip to main content
UDSM na UH

UDSM na UH vyafanikisha upatikanaji wa Kamusi ya Kihispania-Kiswahili

Na Mwandishi Wetu, CMU

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Havana(UH), Cuba kimefanikisha uandaaji wa Kamusi ya Kihispania-Kiswahili, ambayo imezinduliwa tarehe 8 Novemba, 2024, Jijini Havana, Cuba.

Kamusi hiyo ya Kihistoria, imezinduliwa kwenye Kongamano la Kimataifa la Kiswahili ambalo linaendelea Jijini Havana nchini Cuba  kuanzia tarehe  7 hadi 11 Novemba, 2024.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kamusi hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Kongamano hilo la Kiswahili alisema ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Havana katika kukuza Kiswahili utasaidia wananchi wa pande zote mbili kunufaika kupitia wataalamu wa vyuo hivyo.

“Hii ni hatua kubwa na  ya kujivunia kwani itasaidia wenzetu wa Cuba kujifunza Kiswahili kwa wingi zaidi na hivyo kuongeza idadi ya watumiaji wa Lugha hii duniani,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Viongozi wengine waliohudhuria Kongamano hilo pamoja na Waziri, Dkt. Ndumbaro, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kuba Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, na Mhe. Tabia Maulid Mwita - Waziri wa Habari, Vijana, Utamadauni na Michezo wa Zanzibar ambaye amefunga Kongamano hilo.

Ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika tukio hilo uliongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Prof Bonaventure Rutinwa.

Prof. Rutinwa na ujumbe wa UDSM, akiwemo Prof. Shani Omari Mchepange, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, UDSM, wamempongeza Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole kwa Kongamano hilo na kuwa Chuo kinaunga mkono juhudi za kulifanya kuwa endelevu.

Kongamano la Kiswahili la Kimataifa nchini Cuba limeandaliwa na Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini Cuba na linahudhuriwa  na washiriki zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali duniani.